Victoria Kimani Aingia Soko la Afro House na Wimbo Mpya ‘Joy’

VICTORIA KIMANI AVUKA MIPAKA NA KUIVUSHA SAUTI YA KENYA DUNIANI KUPITIA WIMBO WA AFRO HOUSE ‘JOY’
Nyota wa muziki wa Afropop kutoka Kenya, Victoria Kimani, aungana na watayarishaji wa muziki kutoka Zimbabwe, Dr. Feel na DJ Stavo, katika wimbo mpya unaotarajiwa kuwa sehemu ya albamu mkusanyiko ya kimataifa ya Inner Visions, itakayotoka Novemba 27, 2026.
JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI, Oktoba 12, 2026: Mwanamuziki wa Kenya, Victoria Kimani, anafungua ukurasa mpya katika safari yake ya kimuziki baada ya kuingia rasmi katika ulimwengu wa Afro House na Afro Tech kupitia wimbo mpya unaoitwa Joy, akishirikiana na watayarishaji wa muziki kutoka Zimbabwe, Dr. Feel na DJ Stavo.
Kimani, anayefahamika kwa sauti yake ya kipekee, muziki unaochanganya Afropop na R&B, pamoja na wimbo wake Safari, ni miongoni mwa wasanii wa Kenya waliofanikiwa kujenga jina nje ya mipaka ya nchi yao. Uwezo wake wa utunzi pia uliwahi kumfanya Recording Academy, taasisi inayoratibu tuzo za Grammy, kumtaja kama “Kenya’s Best Kept Secret” — yaani, kipaji cha Kenya ambacho hakijapata kutambuliwa kikamilifu na dunia.
Sasa, kupitia Joy, Kimani anapanua wigo wake wa kimuziki kwa kuingia katika aina ya muziki wa kielektroniki unaozidi kupata umaarufu katika vilabu, majukwaa ya utiririshaji wa muziki na tamasha mbalimbali duniani.
Wimbo huo ni sehemu ya Inner Visions, mradi wa kimataifa wa Afro House uliobuniwa na kuratibiwa na DJ na mtayarishaji wa muziki kutoka Zimbabwe, Dr. Feel. Mradi huo unawakutanisha wasanii, ma-DJ na watayarishaji 16 kutoka Zimbabwe kwa lengo la kuonyesha uwezo wa muziki wa nchi hiyo na kuufikisha kwa hadhira ya kimataifa.
Inner Visions inatarajiwa kutolewa rasmi Novemba 27, 2026, kupitia lebo ya muziki wa Afro House ya Mansa Musa, inayopatikana Afrika Kusini.
Kwa Kimani, ushiriki wake katika mradi huu ni zaidi ya kushirikishwa kwenye wimbo mmoja. Ni fursa ya kuunganisha misingi yake ya Afropop na R&B na sauti za Afro House, huku akipanua ushawishi wake katika soko la muziki wa kimataifa.
AFRO HOUSE YAZIDI KUTIKISA SOKO LA MUZIKI DUNIANI
Ushiriki wa Kimani unakuja wakati Afro House ikizidi kupata nguvu katika tasnia ya muziki wa kielektroniki duniani.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotajwa katika taarifa ya MIDiA Research na Splice ya Januari 2026, Afro House ilitajwa kuwa aina ya muziki iliyofanya vizuri zaidi kwa mwaka huo, baada ya idadi ya upakuaji wake kuongezeka kwa asilimia 778, kutoka 760,355 mwaka 2024 hadi 6,674,943 mwaka 2025.
Ukuaji huo uliifanya Afro House kuwa aina ya pili ya muziki iliyopakuliwa zaidi kupitia Splice na kuchangia takribani asilimia 70 ya ukuaji wote wa muziki wa House kwenye jukwaa hilo.
Katika jukwaa la Beatport, Afro House nayo ilipanda kutoka nafasi ya 23 hadi nafasi ya nne katika orodha ya aina za muziki zilizotafutwa zaidi.
Mwelekeo huo unaonekana pia katika mafanikio ya wasanii wanaovuka mipaka ya aina za muziki. Wimbo Move, uliotayarishwa na Adam Port na kundi la Keinemusik kwa kushirikiana na Camila Cabello, ulivuka jumla ya mitiririko milioni 74 kwenye Spotify na kuingia katika chati ya Billboard Global 200.
Kwa upande wa biashara, soko la muziki wa kielektroniki duniani lilifikia thamani ya rekodi ya dola bilioni 15.1 mwaka 2025, likiwa limeongezeka kwa asilimia saba ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Wakati huohuo, mapato ya muziki uliorekodiwa katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara yaliongezeka kwa asilimia 22.6 mwaka 2024, na kuvuka dola milioni 110 za Marekani kwa mara ya kwanza.
Ukuaji huu unaonyesha nafasi inayozidi kujitokeza kwa muziki wa Kiafrika katika uchumi wa kimataifa wa burudani, huku Afro House ikiwa miongoni mwa aina za muziki zinazovutia wasikilizaji wapya katika masoko mbalimbali.
AFRIKA MASHARIKI YAENDELEA KUPANUA USHAWISHI WAKE
Mafanikio ya Afro House si jambo geni kwa Afrika Mashariki. Wasanii kutoka eneo hili wameendelea kuonyesha kuwa midundo na lugha za Kiafrika zinaweza kuvuka mipaka na kufikia hadhira ya kimataifa.
Mwimbaji wa Afro House kutoka Kenya, Idd Aziz, aliweka jina lake katika ramani ya kimataifa kupitia sauti yake inayochanganya mitindo ya Kiafrika na muziki wa kisasa wa kielektroniki. Muziki wake umepata nafasi katika majukwaa mbalimbali, kuanzia Nairobi hadi Berlin, Bali na Lisbon.
Vilevile, wimbo Mwaki wa Sofiya Nzau, ulioimbwa kwa lugha ya Kikuyu, ulipata umaarufu mkubwa katika majukwaa ya utiririshaji wa muziki na katika vilabu vya kimataifa.
Sasa, kuingia kwa Victoria Kimani katika ulimwengu wa Afro House kupitia Joy kunaongeza sura nyingine katika safari hiyo.
Tofauti na baadhi ya wasanii wanaojulikana zaidi kwa muziki wa kielektroniki, Kimani anakuja na uzoefu wa Afropop, R&B na utunzi wa nyimbo. Mchanganyiko huo unampa nafasi ya kuunganisha hadhira inayomfahamu kupitia muziki wa pop na wasikilizaji wanaovutiwa na Afro House.
‘JOY’: MCHANGANYIKO WA AFROPOP, R&B NA AFRO HOUSE
Katika wimbo Joy, Kimani amehusika katika utunzi na uimbaji wa sehemu kuu ya sauti, inayojulikana kama topline, pamoja na sauti zinazoongoza wimbo huo.
Mtindo wake wa Afropop na R&B unaunganishwa na utayarishaji wa muziki wa Afro House wa Dr. Feel na DJ Stavo, na kuunda nafasi ya kimuziki inayomruhusu kujaribu mwelekeo mpya bila kuacha utambulisho wake wa kisanii.
Ushirikiano huo pia unaonyesha namna wasanii wa Afrika wanavyoweza kutumia uzoefu wao tofauti kuunda muziki unaoweza kueleweka katika masoko mbalimbali.
Kwa upande wa Kimani, Joy ni fursa ya kuonyesha uwezo wake wa kubadilika kimuziki na kushiriki katika maendeleo ya aina ya muziki inayozidi kupata mashabiki duniani.
DR. FEEL: DARASA LA UZOEFU KATIKA MUZIKI WA KIELEKTRONIKI
Dr. Feel ni mmoja wa watu muhimu nyuma ya mradi wa Inner Visions. Mtayarishaji huyo wa Zimbabwe, anayeishi Afrika Kusini, amejenga uzoefu mkubwa katika muziki wa kielektroniki kupitia utayarishaji wa zaidi ya nyimbo 200, EP zaidi ya 10 na albamu mbili, Made in Africa na Indalo.
Safari yake ya kimataifa imemfikisha katika majukwaa na matukio mbalimbali ya muziki, yakiwemo Sondela Summer Party, Badbox & Friends jijini London, Cé La Vi jijini Dubai na Amsterdam Dance Event.
Pia ameshiriki maonesho katika nchi mbalimbali, zikiwemo Uingereza, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa, Kenya, Cyprus, Zambia na Afrika Kusini.
Uzoefu huo wa kimataifa ni sehemu ya msingi wa Inner Visions, mradi unaolenga kuunganisha vipaji vya Zimbabwe na fursa za muziki katika masoko ya nje.
DJ STAVO: MWANAMUZIKI ANAYEENDELEZA SAUTI YA AFRO HOUSE YA ZIMBABWE
DJ Stavo, aliyezaliwa na kukulia KweKwe, Zimbabwe, anatajwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa sauti ya Afro House ya Zimbabwe.
Mtindo wake wa muziki unaunganisha Organic House na midundo ya asili ya Kiafrika, ala za mapigo, midundo ya ngoma na melodi zinazounda sauti yenye utambulisho wa kipekee.
Akiwa na uzoefu wa miongo kadhaa, DJ Stavo amefanya kazi na majina mbalimbali katika muziki wa Afrika, yakiwemo Mandoza, Shota, Fiesta Black, Trademark, marehemu Dkt. Oliver Mtukudzi, Jah Prayzah, DJ Maphorisa, Di Buckz, Roki na Lady Du.
Miongoni mwa nyimbo zake zinazojulikana ni Simudza Ngoma, Sexy Darling na The Journey. Baadhi ya kazi hizo zimevuka watazamaji milioni moja kwenye YouTube.
Pia amefanya maonesho katika nchi mbalimbali, zikiwemo Afrika Kusini, Msumbiji, Malawi, Botswana, Uingereza na Ugiriki.
Ushiriki wake katika Inner Visions unaongeza uzoefu wa muziki wa Kiafrika katika mradi unaolenga kuunganisha sauti za Zimbabwe na hadhira ya kimataifa.
INNER VISIONS YAKUTANISHA VIPAJI 16 VYA ZIMBABWE
Mbali na Victoria Kimani, mradi wa Inner Visions unajumuisha wasanii na watayarishaji wengine 15 kutoka Zimbabwe na mtandao mpana wa muziki wa Afro House.
Miongoni mwa majina yaliyotajwa ni Nitefreak, Dr. Chaii, Ryan Synth, MIčI, Reverb, TAPIWA, Simbai, Tashinga, Shona (SA), PA NGU, Afro Wav, Takue SBT, Josh Major, Daphfinee na Taarof Adder.
Kwa mujibu wa Tendai Joe, meneja wa mahusiano ya umma na mawasiliano wa mradi huo, ushiriki wa Kimani unaonyesha matokeo yanayoweza kupatikana pale wasanii wa Afrika wanapounganisha vipaji na mitazamo yao kutoka maeneo tofauti.
“Naona huu ni mradi wa kusisimua sana. Kumwona msanii kama Victoria Kimani akiingiza ladha na ushawishi wa Afrika Mashariki katika mchanganyiko huu ni ushahidi wa kile ambacho Afrika inaweza kufanikisha wasanii wake wanapoungana,” alisema Joe.
Aliongeza kuwa Kimani ana uzoefu wa kitaaluma na uhusiano wa kimuziki na majina mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo DJ Whoo Kid, Jadakiss, DJ Green Lantern, Busta Rhymes na Timbaland.
“Kwangu mimi, hicho ndicho kinachoufanya mradi kama Inner Visions kuwa wa kusisimua. Unaonyesha kile kinachowezekana pale wasanii wanapovuka mipaka, kuunganisha ushawishi wao tofauti na kuunda kitu kinachoweza kufika kwa hadhira ya dunia nzima,” alieleza.
Joe pia alibainisha kuwa mkusanyiko huo unawajumuisha watayarishaji wenye uzoefu mkubwa katika soko la kimataifa la muziki.
Alimtaja Nitefreak, ambaye kazi zake mbili zimekusanya zaidi ya mitiririko milioni 100 kwa pamoja kwenye Spotify, kuwa miongoni mwa majina muhimu katika mradi huo. Aliongeza kuwa msanii huyo amewahi kufanya maonesho nchini Kenya, jambo linalomfanya afahamike kwa baadhi ya mashabiki wa muziki wa Nairobi.
Aidha, Joe alimtaja Dr. Chaii, mtayarishaji wa muziki mwenye asili ya Zimbabwe anayeishi Los Angeles, Marekani, ambaye ameteuliwa mara tano kuwania tuzo za Grammy.
Kwa mujibu wa Joe, Dr. Chaii amefanya kazi na wasanii wa kimataifa wakiwemo Tyla, Dua Lipa, Sean Paul, Chris Brown, Pitbull, J Balvin, Maroon 5, Inna, Camila Cabello, Blondish na Nicki Minaj.
Pia amehusika katika utayarishaji wa sauti kwa filamu kama Fast & Furious, Spider-Man: Into the Spider-Verse na Baywatch, pamoja na kazi za televisheni zinazohusishwa na NFL na Netflix.
Kwa Joe, uwepo wa majina haya unaonyesha upana wa vipaji na uzoefu unaokutana katika Inner Visions.
LENGO NI KUIPELEKA MUZIKI WA ZIMBABWE KWENYE RAMANI YA DUNIA
Joe alisema kuwa Inner Visions haijalenga tu kuangazia mafanikio ya msanii mmoja mmoja, bali pia kujenga jukwaa litakalosaidia kukuza tasnia nzima ya muziki wa Zimbabwe.
Kwa mujibu wake, mradi huo unalenga kuongeza mwonekano wa wasanii wa Zimbabwe, kuimarisha ushirikiano wa kikazi na kufungua njia mpya za kuifikisha muziki wa House wa nchi hiyo kwa wasikilizaji wa kimataifa.
Kupitia ushirikiano wa wasanii kutoka mataifa tofauti, mradi huo unatarajia kuonyesha namna muziki unavyoweza kuwa daraja la kuunganisha tamaduni, kukuza vipaji na kuunda fursa mpya za kibiashara.
Ushirikiano wa Kimani na watayarishaji hao unaongeza mwelekeo wa Afrika Mashariki katika juhudi hizo, huku ukionyesha uwezekano wa wasanii wa Kenya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Afro House na Afro Tech.
‘JOY’ YAWEKA AFRIKA MASHARIKI KATIKA MAZUNGUMZO YA AFRO HOUSE
Kwa mashabiki wa muziki Afrika Mashariki, ushiriki wa Kimani katika Joy unaashiria fursa mpya kwa wasanii wa eneo hili kushirikiana na watayarishaji wa muziki wa kielektroniki kutoka sehemu nyingine za bara.
Afro House na Afro Tech si mitindo ya muziki inayopaswa kuonekana kuwa mali ya masoko ya mbali pekee. Ni maeneo ambayo wasanii wa Kenya na mataifa mengine ya Afrika Mashariki wanaweza kushirikiana, kujaribu sauti mpya na kufikia hadhira pana zaidi.
Kwa Kimani, hatua hii inatoa nafasi ya kupanua upeo wake wa kisanii. Kwa Dr. Feel na DJ Stavo, inafungua mlango wa kuunganisha mradi wao na hadhira inayomfahamu Kimani kupitia kazi zake za Afropop na R&B.
Na kwa Inner Visions, ushirikiano huo unatoa mfano wa namna vipaji kutoka sehemu mbalimbali za Afrika vinavyoweza kuungana na kutengeneza muziki unaovuka mipaka ya kijiografia na kimtindo.
Huku mashabiki wakisubiri kusikiliza wimbo huo, macho yanaelekezwa kwenye Novemba 27, 2026, siku ambayo Inner Visions inatarajiwa kutolewa rasmi kupitia lebo ya Mansa Musa.
Kwa sasa, ‘Joy’ bado haijatolewa rasmi kwa umma.
KUHUSU INNER VISIONS
Inner Visions ni mradi wa kimataifa wa Afro House ulioanzishwa na kuratibiwa na DJ na mtayarishaji wa muziki kutoka Zimbabwe, Dr. Feel. Unawakutanisha ma-DJ, watayarishaji na wasanii 16 kutoka Zimbabwe kwa lengo la kuonyesha vipaji vya nchi hiyo kwa hadhira ya kimataifa kupitia ushirikiano, kuongeza mwonekano wa wasanii na kukuza muziki wa Afro House duniani.
KUHUSU VICTORIA KIMANI
Victoria Kimani ni mwimbaji, mtunzi wa nyimbo na mburudishaji kutoka Kenya anayejulikana kwa muziki wake unaochanganya Afropop na R&B. Akiwa na albamu tano za studio na ushirikiano mbalimbali wa kimataifa, Kimani anaendelea kupanua wigo wa muziki wake na kuchangia katika kuutambulisha muziki wa Kenya kwa hadhira ya kimataifa.
KUHUSU DR. FEEL
Dr. Feel ni DJ na mtayarishaji wa muziki kutoka Zimbabwe anayeishi Afrika Kusini. Ana zaidi ya nyimbo 200, EP zaidi ya 10 na albamu mbili, Made in Africa na Indalo. Kazi zake zimetolewa kupitia lebo mbalimbali za kimataifa, zikiwemo Defected, Sondela, Deep Root Tribe, Nervous na Aluku. Anaendelea kujenga uhusiano kati ya muziki wa kielektroniki wa Afrika na tasnia ya muziki wa dansi duniani.
KUHUSU DJ STAVO
DJ Stavo ni DJ, mtayarishaji wa muziki wa kielektroniki na remixer kutoka Zimbabwe, aliyezaliwa na kukulia KweKwe. Anajulikana kwa mchango wake katika kuendeleza sauti ya Afro House ya Zimbabwe, akichanganya Organic House na midundo ya asili ya Kiafrika, melodi, mapigo na ngoma.
Katika safari yake ya miongo kadhaa, amefanya kazi na wasanii mbalimbali wakiwemo Mandoza, Shota, Fiesta Black, Trademark, marehemu Dkt. Oliver Mtukudzi, Jah Prayzah, DJ Maphorisa, Di Buckz, Roki na Lady Du.
Nyimbo zake zinazojulikana ni pamoja na Simudza Ngoma, Sexy Darling na The Journey, ambazo baadhi yake zimevuka watazamaji milioni moja kwenye YouTube. Ameshinda tuzo mbalimbali na kufanya maonesho katika Afrika Kusini, Msumbiji, Malawi, Botswana, Uingereza na Ugiriki.
RELATED:
- Diamond Platnumz: Jinsi Alivyobadilisha Bongo Flava Kuwa Biashara ya Kimataifa
- Diamond Platnumz: Msanii Anayebadilisha Tukio Lake Kuwa Big Story ya Tanzania
- TOP 10 Best Songs of ZUCHU Of All Time (Nyimbo 10 Bora Za Zuchu za Muda Wote)
- Zuchu Imbeju Masterclass 2026 Yatikisa Tanzania!
- Big News: Zuchu Kapata Mtoto wa Kike na Diamond Platnumz?
- Top 20 za Nyimbo Bora za Bongo Flava za Muda Wote (Orodha Kamili 2026)




