Rasim: Mbwana Samatta Atangaza Kustafu kuitumikia Timu ya Taifa Star Kabla Ya Afcon 2027
Rasmi: Mbwana Samatta Atangaza Kustafu Kuitumikia Timu ya Taifa Stars Kabla ya AFCON 2027
Nahodha wa muda mrefu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta, ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia Taifa Stars, akihitimisha safari yake ya takribani miaka 15 akiwa mchezaji wa timu hiyo.
Kupitia taarifa aliyochapisha, Samatta amesema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, akieleza kuwa anajivunia kipindi alichokitumikia Taifa Stars na kushukuru kwa nafasi aliyopata ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Samatta amesema miaka 10 aliyokuwa nahodha wa Taifa Stars imekuwa sehemu muhimu ya maisha yake ya soka. Katika kipindi hicho, aliiongoza Tanzania kufuzu Fainali za AFCON mara tatu na pia kushuhudia historia ikipekwa kwa Taifa Stars kwa kufuzu hatua ya 16 bora ya AFCON kwa mara ya kwanza.
Aidha, amesema anaamini sasa ni wakati wa kutoa nafasi kwa kizazi kipya cha wachezaji kuendelea kuijenga timu na kufikisha mafanikio makubwa zaidi katika miaka ijayo.
Katika ujumbe wake, Samatta ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), makocha, viongozi, wachezaji wenzake, familia yake pamoja na Watanzania wote waliomuunga mkono katika safari yake ya kuitumikia Taifa Stars.
Pia amesisitiza kuwa, licha ya kustaafu kuchezea Timu ya Taifa, ataendelea kutoa mchango wake kwa maendeleo ya soka la Tanzania kupitia uzoefu na uwezo wake katika nyanja nyingine.
Kustaafu kwa Mbwana Samatta kunakuja wakati Tanzania ikiwa inaendelea na maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, ambayo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zitakazoandaa kwa ushirikiano na Kenya na Uganda.
Tunamtakia kila la heri Mbwana Samatta katika hatua mpya ya maisha yake na tunamshukuru kwa mchango mkubwa alioutoa kwa Taifa Stars na soka la Tanzania kwa ujumla.

Related Articles:

